Mkutano wa Nairobi waunga mkono mpango mpya wa China wa GGI kusaidia nchi zinazoendelea

Mjumbe wa Ubalozi wa China na wasomi wa Kenya wasema mfumo huu mpya unatoa haki, ujumuishi na sauti yenye nguvu zaidi kwa mataifa yanayoendelea katika masuala ya kimataifa.

Eric Biegon
5 Min Read
Kaimu Balozi wa China nchini Kenya, Zhang Zhizhong

Pendekezo mpya la China la utawala wa dunia  maarufu kama GGI umepongezwa kama jibu la wakati muafaka kwa hali ya sasa duniani na kama njia ya kuongeza ushawishi wa nchi za kusini mwa dunia.

Akizungumza wakati wa mkutano uliofanyika jijini Nairobi, Kaimu Balozi wa China nchini Kenya, Zhang Zhizhong, pamoja na wasomi mashuhuri wa Kenya walisisitiza uwezo wa mpango huo kuunda upya uhusiano wa kimataifa kwa misingi ya haki, ushirikiano na ustawi wa pamoja.

“Kutokuwa na utulivu, kutokuwa na uhakika na kutotabirika kumegeuka kuwa hali ya kawaida,” alisema Bwana Zhang katika hotuba yake kuu.

“Inazidi kuwa vigumu kueleza dunia ya leo na kutatua changamoto kwa kutumia nadharia za jadi za uhusiano wa kimataifa. Ndiyo maana Rais Xi Jinping alipendekeza kujenga jamii yenye mustakabali wa pamoja kwa wanadamu wote,” alieleza.

Bwana Zhang alibainisha kuwa GGI inakamilisha mipango mingine mitatu inayosukumwa na China, ambazo ni: Mpango wa Maendeleo ya dunia (GDI), Mpango wa Usalama wa Kidunia (GSI), na Mpango wa Ustaarabu wa Kidunia (GCI) ambazo zote zinaimarishana kwa kuingiza “utulivu na uhakika katika dunia yenye misukosuko.”

Aliongeza kuwa GGI hailengi kubomoa mfumo wa sasa wa kimataifa bali kurekebisha “mipangilio isiyo ya haki na isiyofaa katika mfumo wa sasa wa utawala wa dunia,” jambo ambalo “linawiana na maslahi ya msingi ya nchi za kusini mwa dunia, ikiwemo Kenya.”

“China iko tayari kushirikiana na Kenya na pia na nchi nyingine za kusini mwa dunia kuendesha ushirikiano wa mfano katika kuendeleza GGI,” alisema.

Mchumi wa Kenya na Mkurugenzi wa Inter Region Economic Network, James Shikwati, alielezea GGI na mipango mingine kutoka China kama fursa kwa Afrika kujiondoa kwenye utegemezi wa miundo ya sasa ya kimataifa.

“China inatufungulia macho kuhusu uwezekano wa mfumo wa dunia baada ya miaka 500 ya utawala wa Magharibi, ikitupatia njia mbadala wa maendeleo, usalama kama kanuni kuu ya uendeshaji, utamaduni kama mshikamano na mageuzi ya utawala kama mfumo wa kufanya kazi,” alisema.

Alitaja reli ya kisasa ya SGR na mitandao ya barabara nchini Kenya kama matunda ya mtazamo wa miradi chini ya mpango wa maendeleo ya dunia (GDI). Pia aliongeza kuwa uamuzi wa hivi karibuni wa China wa kupanua upatikanaji wa bidhaa bila ushuru kwa nchi za Afrika unaonyesha dhamira ya Beijing ya haki ya kibiashara kwa bara hili.

“Kwa Kenya na Afrika, hii ni fursa ya kubadilisha biashara, kupunguza hatari katika njia kuu za kibiashara, na kukumbatia mageuzi ya utawala jumuishi ambayo hatimaye yanazipa nchi za kusini mwa dunia sauti katika masuala ya fedha, teknolojia na mabadiliko ya tabianchi,” alisema Shikwati.

Profesa Patrick Maluki, mwenyekiti wa idara ya diplomasia na masomo ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Nairobi, alisisitiza kuwa mpango huu unakuja kwa wakati ambapo “utawala wa dunia lazima ujengwe juu ya haki, usawa, ushirikiano na heshima ya pande zote.”

“Mpango huu mpya wa utawala wa dunia (GGI) unasisitiza mazungumzo badala ya migongano, ushirikiano badala ya ushindani wa sifuri, na uwajibikaji wa pamoja badala ya utawala wa upande mmoja,” alisema.

Kwa upande wake, Dkt. Mutinda Mutisya, Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa China cha Afrika katika Chuo Kikuu cha Nairobi, alihusisha GGI na mshikamano wa kihistoria kati ya China na Afrika katika kupinga ukoloni na uvamizi.

“Hadithi ya China na Afrika ni ya ujasiri, ustahimilivu na hatima ya pamoja. Inatulazimisha kuchukua hatua, kushirikiana na kubaki thabiti katika kutafuta haki na heshima,” alisema.

“Mshikamano ni zaidi ya maneno ya mdomo, kwani ni ahadi ya utekelezaji inayohitaji ujasiri, maono na juhudi za kudumu,” aliongeza.

Washiriki walikubaliana kuwa mpango huu umewadia kwa wakati ufaao. Dunia ikikabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, ushindani wa kisiasa, ukosefu wa usawa wa kifedha na msukosuko wa kiteknolojia, walieleza kuwa mapendekezo ya China yanatoa njia mahsusi kwa mataifa ya kusini mwa dunia kushiriki kikamilifu katika kutafuta suluhu badala ya kusubiri maamuzi kutoka kwingine.

“Kwa Kenya na Afrika, huu ni mpango bora wa mageuzi katika masuala ya fedha, madeni, viwango vya biashara, utawala wa kidijitali / akili mnemba na mifumo ya tabianchi ili kuingiza sauti za Kusini mwa Dunia,” alihitimisha Shikwati.

Mkutano huu ulimalizika kwa mwito wa kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya China na Kenya, pamoja na China na Afrika kwa ujumla, ili kuendeleza GGI na mipango mingine inayohusiana nayo.

Share This Article