Mkurugenzi wa DCI Mohamed Amin atakiwa kufika Mahakamani

Tom Mathinji
1 Min Read
Mkurugenzi wa idara ya DCI Mohamed Amin.

Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Mohamed Amin, ametakiwa kufika katika Mahakama Kuu Nairobi siku ya Alhamisi, kuelezea aliko mwanablogu Ndiang’ui Kinyagia.

Akitoa agizo hilo, Jaji  Chacha Mwita alisema maafisa kutoka idara hiyo ya upelelezi, walikuwa watu wa mwisho kuzuru nyumbani kwake mwanablogu huyo kabla  ya kutoweka kwake.

Jaji Mwita alidokeza kuwa mahakama inataka ufafanuzi kutoka kwa Amin kuhusu aliko mwanablogu Kinyagia, huku akitakiwa na mahakama hiyo lazima awajibikie vitendo vya idara hiyo.

Aidha, Jaji huyo pia aliwaagiza  Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, na  Mkurugenzi wa DCI Mohamed  Amin kumwasilisha mwanablogu huyo akiwa hai au akiwa ameaga dunia. Jaji  Mwita alitaka kesi hiyo itajwe  Alhamis asubuhi.

Agizo hilo linafuatia wasiwasi kuhusiana na aliko mwanablogu huyo baada ya kutoweka  kwa muda wa zaidi ya  siku kumi.

Agizo hilo la mahakama linajiri huku kukiwa na madai  kutoka kwa serikali kupitia hati ya kiapo ya sajenti  Samuel Itegi wa idara ya upelelezi – DCI, kwamba  Kinyagia anachunguzwa kwa madai ya uchochezi wakati wa maandamano ya vijana wa kizazi cha Gen Z.

Share This Article