Mwendeshaji baiskeli wa Kenya Benson Mwaniki amejiondoa kwa mashindano ya Olimpiki ya Walemavu yaliyoratibiwa kung’oa nanga kesho kutwa jijini Paris nchini Ufaransa baada kujeruhiwa kwenye ajali wiki jana.
Mwaniki amelazimika kujiondoa baada ya kujeruhiwa wiki jana na kuumia bega na uti wa mgongo, baada ya kugongwa na gari akiwa njiani kuelekea mazoezini Compiegne nchini Ufaransa.
Mwaniki, alikuwa awe mwelekezi wa mwendeshaji mlemavu Kennedy Ogada lakini kulingana na ripoti ya matabibu, atahitaji angalau wiki sita kupona majeraha hayo ya ajali.
Licha ya ajali hiyo, Ogada angali na imani ya kutwaa medali endapo atapata mwelekezi mwingine kwa muda ufaao.
Kiongozi wa ujumbe wa Kenya kwa michezo hiyo Dennis Muga amesema kuwa kamati ya Olimpiki kwa Walemavu (KNPC), imeanza mchakato wa kumtafuta mwendeshaji mbadala atakayetwaa nafasi ya Mwaniki.
Ogada ambaye ni mlemavu asiyeona anatarajiwa kushiriki mashindanoni Septemba 4 katika kitengo cha B1.