Mkakati wa kuwekeza pesa za ughaibuni wazinduliwa

Marion Bosire
2 Min Read

Waziri aliye na mamlaka makuu Musalia Mudavadi ambaye pia ni waziri wa mambo ya nje na masuala ya ughaibuni, jana Jumanne aliongoza uzinduzi wa mkakati wa uwekezaji wa wa pesa zinazotumwa Kenya kutoka ughaibuni wa mwaka 2025 hadi 2030.

Hafla hiyo ilitumika pia kuzindua toleo jipya la kijitabu kuhusu utoaji wa kidijitali hatua ambazo alizitaja kuwa ishara ya mwelekeo mpya na thabiti, katika jinsi nchi inavyoshirikiana na Wakenya wanaoishi nje ya mipaka.

Mudavadi alisema mkakati huo mpya unatoa ramani inayoeleweka na ya vitendo ya kubadilishapesa zinazotoka ughaibuni kutoka kuwa msaada wa muda mfupi kwa familia hadi kuwa uwekezaji wa muda mrefu unaozalisha utajiri.

Mpango huo unaainisha fursa za uwekezaji katika makazi, miundombinu, viwanda na ubunifu, kwa lengo la kuwapa Wakenya waishio ughaibuni ujasiri zaidi wa kuelekeza rasilimali zao katika miradi inayojenga thamani ya kudumu kwa jamii na taifa.

Kijitabu hicho kuhusu uwasilishaji wa pesa kidijitali, kilichoandaliwa kwa ushirikiano na IOM Kenya na wadau wengine, kinatolewa kama mwongozo rahisi kwa Wakenya walio nje kuhusu jinsi ya kutuma pesa salama na kusimamia fedha zao kwa njia ya mbali.

Kinaeleza pia kuhusu njia salama, mbinu za kidijitali na mbinu za kupunguza gharama ili kufanya miamala kuwa salama zaidi, wazi na yenye ufanisi.

Mudavadi alisema hatua hizi mbili zimekusudiwa kujenga upya imani, kupanua njia za uwekezaji na kuwezesha Wakenya wa ughaibuni kuchukua jukumu muhimu zaidi katika mageuzi ya kijamii na kiuchumi ya Kenya.

“Tunapoadhimisha hatua hii muhimu, narudia kusisitiza kwamba Wakenya walio ughaibuni sio wachangiaji tu wa simulizi la taifa; ni washirika wakuu katika kujenga Kenya yenye ukuaji wa pamoja, fursa na ustawi kwa wote,” alisema.

Share This Article