Mjane wa mwanamuziki wa Nigeria Mohbad aitwaye Wunmi Cynthia Aloba, amekubali kwamba atamfanyia mwanawe vipimo vya msimbojeni almaarufu DNA.
Katika mahojiano na BBC Pidgin, Wunmi alisema kwamba anakubali hitaji la babake Mohbad Joseph Aloba aliyetaka kufahamu iwapo marehemu mwanawe ndiye baba halisi wa mtoto huyo.
Lakini tena Wunmi alifafanua kwamba hafanyi vipimo hivyo kumridhisha baba mkwe kwani ana uhakika kwamba Liam ni mjukuu wake halisi.
Anasema anafanya vipimo hivyo vya DNA ili watu wa Nigeria waridhike na hivyo kukomesha mashaka yao kuhusu baba halisi ya mtoto huyo.
Liam alizaliwa Februari 22, 2023.
Wunmi alisema kwamba anamkumbuka aliyekuwa mume wake, anakosa sana kila jambo kumhusu na kila mara anapomzungumzia anazidiwa na hisia.
Alisema alipompeleka mtoto huyo shuleni, majina ya wazazi wake yalinakiliwa kama bwana na bi Aloba hatua iliyomridhisha.
Mohbad ambaye jina lake halisi ni Ilerioluwa Oladimeji Aloba, alifariki kwa njia ya kutatanisha Septemba 12, 2023, akiwa na umri wa miaka 27.
kifo chake kilichotokea jijini Lagos nchini Nigeria kilighubikwa na utata lakini uchunguzi wa maiti ulibaini kwamba alifariki kutokana na majeraha aliyopata alipopigana na rafiki yake Ibrahim Owoduni maarufu kama Prime Boy.
Muuguzi kwa jina Fisayo Ogedengbe, alikuwa akimtibu Mohbad kutokana na majeraha hayo nyumbani na dawa alizompa zikasababisha matatizo kama kutapika na kuzirai na hivyo kusababisha kifo chake.