Ziara ya hivi majuzi ya kundi la wazee wanaomuunga mkono Spika wa Bunge la Kaunti ya Isiolo aliyeondolewa ofisini kwa njia tata, Mohamed Roba Qoto, katika Ikulu ya Nairobi imezua tafrani kubwa ya kisiasa katika kaunti ya Isiolo.
Viongozi wanaomuunga mkono Gavana Abdi Guyo wameikosoa ziara hiyo, wakidai kwamba ujumbe huo ulitanguliza maslahi yao binafsi ya kisiasa badala ya maslahi ya wakazi wa Isiolo.
Rais William Ruto alikutana na kundi hilo Jumatano juma lililopita, wiki chache tu baada ya Seneti kukatiza jaribio la kumng’oa Gavana Guyo mamlakani. Ziara hiyo imechochea zaidi mvutano unaoendelea kuhusu uhalali wa nafasi ya Spika wa Bunge la Kaunti ya Isiolo.
Taarifa tata ya gazeti rasmi la serikali ilitangaza kuondolewa kwa Spika Mohamed Roba Qoto na kumweka aliyekuwa mbunge wa Isiolo Kusini, Abdullahi Banticha Jaldesa, kama mrithi wake. Hata hivyo, suala hilo bado liko mahakamani.
Akizungumza katika mji wa Garbatula katika hafla ya kuwezesha vikundi vya kina mama na vijana, Mwakilishi wa Wanawake wa Isiolo, Mumina Bonaya, alikosoa vikali ujumbe huo, akisema waliupotosha uongozi wa nchi kwa sababu ya misingi ya kisiasa. Alisema hawakutumia fursa hiyo kuwasilisha masuala ya maendeleo kwa ajili ya wakazi wa Isiolo.
Mbunge wa zamani wa Isiolo Kusini, Abdi Koropu Tepo, pia alilaani kundi hilo, akidai walijitambulisha kimakosa kama wawakilishi wa jamii zote za Isiolo ilhali walikuwa wakiwakilisha ukoo mmoja pekee.
Alikanusha madai kwamba Rais Ruto alimrudisha Qoto kama spika, akifafanua kwamba Rais alisisitiza kuwa suala hilo ni lazima litatuliwe kwa mujibu wa sheria.
Abdullahi Banticha, anayeshikilia kwa sasa nafasi ya Spika iliyo na utata, alisema ujumbe uliokutana na Rais haukuwakilisha sauti wala maslahi ya wengi katika kaunti ya Isiolo.
Alimtuhumu aliyekuwa Mwakilishi wa Wanawake, Rehema Dida Jaldesa, kwa kumpa Rais taarifa potofu na kuonya kuwa hatua zake za awali zilisababisha migawanyiko mikubwa ya kisiasa katika eneo hilo.
Wakati hali ya taharuki ikizidi, ziara hiyo ya Ikulu imekuwa mtihani mkubwa wa kisiasa kwa Rais Ruto, ambaye sasa anakabiliwa na shinikizo la kusuluhisha mgogoro wa uongozi unaozidi kutokota Isiolo.
Katika ziara hiyo, vikundi vya wanawake na vijana vilipokea vifaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na mahema, viti, mashine za kuoshea magari pamoja na hundi zenye thamani ya shilingi milioni mbili kutoka kwa Hazina ya Uwezeshaji wa Wanawake ya Serikali Kuu (N.G.A.A.F) inayosimamiwa na afisi ya Mwakilishi wa Wanawake.
Serikali ya kaunti pia ilikabidhi kila kikundi cha wanawake shilingi elfu hamsini (50,000) kama mtaji wa kuanzisha vikundi vya Akiba ya Kijiji, mpango ulioanzishwa na afisi ya Mwakilishi wa Wanawake.