Serikali inatekeleza maendelo ya miundombinu, Ili kuhakikisha ustawi wa taifa hili unatimizwa. Hayo yamesemwa na kiongozi wa taifa Rais William Ruto.
Akizungumza alipoongoza taifa kuadhimisha Siku Kuu ya Mashujaa katika uwanja wa Ithookwe kaunti ya Kitui, Rais alisema kilomita 1,000 za barabara zenye safu mbili zitajengwa kote nchini.
“Barabara hizo ni pamoja na Rironi-Nakuru-Mau Summit-Eldoret-Malaba, Makutano-Embu-Meru, KitengelaNamanga, Mombasa-Nairobi na Marua-Nanyuki-Isiolo,” alisema Rais Ruto.
Wakati huo huo Rais Ruto alidokeza kuwa kilomita 10,0000 za barabara zitawekwa lami ili kuwaunganisha wakulima pamoja na watengenezaji bidhaa na masoko.
Aidha alisema utawala wake utakamilisha ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR kutoka Naivasha hadi Kisumu na kuendelea hadi Malaba, ili kuunganisha taifa hili na Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.
Rais alisema miradi hiyo hutekelezwa na viongozi wajasiri, jinsi alivyokuwa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.