Mwanamuziki wa Uganda Michael Mukwaya maarufu kama Mikie Wine ana kila sababu ya kutabasamu kufuatia mafanikio makubwa aliyoyapata kwenye mauzo ya tiketi za tamasha lake lijalo.
Mikie Wine amefuchua kwamba amefanikiwa kuuza tiketi za meza zote za Platinum za tamasha hilo.
Mwimbaji huyo hangeweza kuficha furaha yake huku akishukuru Mungu na mashabiki zake kwa kumuunga mkono anaposherehekea hatua kubwa maishani mwake.
Kaka huyo wa mwanamuziki na mwanasiasa Bobi Wine alisema, “Mungu amekuwa mwema kwango na meza zote za Platinum zilizokuwa zikiuzwa shilingi milioni 5 zote zimeisha.”
Kulingana naye, meza ambazo zimebaki ni kumi za kiwango cha Gold ambapo kila moja inauzwa shilingi milioni 3, pesa za Uganda.
Mikie ameandaa tamasha hilo kusherehekea miaka 15 katika muziki na litaandaliwa Jumamosi Novemba 15, 2025 katika hoteli ya kifahari ya Serena jijini Kampala.
Msanii huyo ameahidi watakaohudhuria usiku usiosahaulika kutokana na burudani ambayo ameandaa akiwapa miziki mbali mbali aliyotoa katika kipindi cha miaka 15.