Gavana wa zamani wa kaunti ya Nairobi Mike Sonko amejiunga na chama kipya cha National Economic Development, NEDP.
Chama hicho kilikabidhiwa cheti cha usajili leo Jumanne asubuhi katika hafla iliyoongozwa na Msajili wa Vyama vya Kisiasa, John Lorionokou.
Sonko ndiye kiongozi wa chama hicho huku Ben Mulwa akiteuliwa kuwa Katibu Mkuu.
Mulwa alikuwa Mkuu wa Wafanyakazi wakati Sonko alipohudumu kama Gavana.
“Chama hiki kitaunda serikali ijayo na kuongoza mapinduzi ya kiuchumi,” aliahidi Mulwa wakati wa uzinduzi huo.
Uzinduzi wa chama hicho ni ishara inayonukia ya mchipuko wa vyama vya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Tayari, vyama kadhaa vya kisiasa vimeanza kuonyesha dalili ya kuunda miungano ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao unaobashiriwa kuwa wenye ushindani mkali.
Utawala wa Kenya Kwanza ukichumbia chama cha ODM kuelekea uchaguzi huo huku muungano wa upinzani ukiongozwa na kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ukiahidi kufanya kila uwezalo kuifurusha serikali ya sasa madarakani.