Waziri wa Utalii na Wanyamapori Rebecca Miano ametoa wito wa uhifadhi mazingira kupitia upanzi wa miti, akisema mabadiliko ya tabia nchi yameathiri uzalishaji chakula na maziwa.
Miano alisema kuwa wakazi wa Nyandarua hawapati mavuno mengi jinsi ilivyokuwa hapo awali, kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Kulingana na waziri huyo, iwapo uhifadhi mazingira utatekelezwa kupitia upanzi wa miti, kaunti ya Nyandarua itakuwa na uwezo mkubwa wa kuzalisha chakula cha kutosha kwa taifa hili na pia kuuzwa katika masoko ya nje.
“Katika Wizara ya Utalii na Wanyamapori, tunajizatiti kuhakikisha kuwa uhifadhi wa mazingira unawafaidi pakubwa watu wetu,” alisema Waziri Miano.
Waziri huyo aliyasema hayo katika eneo la Tulaga, Kinangop, kaunti ya Nyandarua wakati wa zoezi la upanzi wa miti.
Akiunga mkono matamshi ya waziri huyo, kamishna wa kaunti ya Nyandarua Abdrisack Jaldesa alisema swala la mabadiliko ya tabia nchi ni la kijamii na pia kiuchumi.