Mgomo wa wahadhiri waendelea chuoni Moi

Marion Bosire
1 Min Read

Mgomo wa wahadhiri katika Chuo Kikuu cha Moi umeingia wiki ya tatu, huku mazungumzo kati ya Chama cha Wahadhiri wa Vyuo Vikuu (UASU) na usimamizi wa chuo hicho yakiwa bado hayajazaa matunda.

Naibu Chansela wa chuo hicho Profesa Kiplagat Kotut, ameonyesha matumaini kwamba mkwamo huo unaweza kutatuliwa, akisema kuwa mazungumzo mapya yanapangwa ili kushughulikia masuala yaliyoibuliwa na chama hicho.

Hata hivyo, mazungumzo yaliyofanyika wiki iliyopita kati ya pande hizo mbili yalimalizika bila makubaliano yoyote.

Maafisa wa UASU wakiongozwa na Mwenyekiti Richard Okero wamesisitiza kuwa wanachama wao hawatarejea kazini hadi madai yao yatimizwe.

Aliongeza kuwa chama hicho kimeandika barua kwa usimamizi wa chuo na kwamba mkutano mwingine umepangwa kufanyika leo.

Masomo yamesitishwa kabisa chuoni humo huku UASU ikisisitiza kutekelezwa kwa madai 25, yakiwemo malipo ya malimbikizo ya mishahara na kurejeshwa kwa makato ya kisheria na ya wahusika wa tatu.

Chama hicho kinadai kuwa malimbikizo hayo yanazidi Shilingi bilioni 9.

Katibu wa tawi la UASU, Wegesa Busolo, alisema kuwa ofa iliyotolewa na chuo wakati wa mazungumzo ilikuwa chini sana ya matarajio yao.

Licha ya mkwamo huo, Profesa Kotut ameendelea kusisitiza kuwa chuo kiko tayari kwa mazungumzo na anaamini kuwa makubaliano yanaweza kufikiwa.

Share This Article