Wafanyakazi wa viwanja vya ndege nchini chini ya chama chao KAWU wameahirisha mgomo wao uliokuwa umepangwa kuanza Jumatatu Agosti 19, 2024.
Katika taarifa katibu mkuu wa chama hicho Moss Ndiema alisema kwamba wameahirisha mgomo huo kwa muda wa wiki mbili kutoa fursa kwa mashauriano na serikali, baada ya mkutano wa viongozi wakuu wa KAWU.
Suala kuu lililochochea mgomo huo ni mapatano kati ya serikali na kampuni ya Adani kutoka India ya usimamizi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta JKIA.
Ndiema aliyezungumza na wanahabari jana Jumamosi Agosti 17, 2024, alisema kwamba walialikwa kwa mazungumzo na waziri mpya wa Leba Alfred Mutua Jumatano wiki jana.
Baada ya majadiliano ya muda, waliamua kuahirisha mgomo wao huku majadiliano yakiendelea. Jumanne wiki ijayo watafanya mkutano na waziri wa uchukuzi Davis Chirchir kuhusu suala hilo.
Ndiema anashikilia kwamba hawatakubali uwanja wa JKIA usimamiwe na kampuni ya Adani kwani hatua hiyo huenda ikaathiri ajira ya wanachama wa KAWU wapatao elfu moja.
Wafanyakazi wa JKIA wanalalamika kwamba hawakufahamishwa kuhusu mabadiliko katika usimamizi na waliona taarifa hizo mitandaoni.
Wanahisi kwamba iwapo Adani itachukua usimamizi wa JKIA, watafutwa kazi na kulazimika kuomba tena upya nafasi zao za kazi na hakuna hakikisho kwamba wataajiriwa tena.
Watakaoajiriwa na Adani wataajiriwa kwa masharti duni sula ambalo wamesema hawatakubali.