Serikali ya Uganda kupitia kwa wizara ya uchukuzi imesimamisha matumizi ya mfumo wa kielektrokini wa kutambua wanaokiuka sheria za trafiki na kuwatoza faini kufuatia lalama za umma.
Kupitia mtandao wa X, wizara hiyo ilisema kwamba mfumo huo umesimamishwa kwa muda baada ya utathmini wa kina.
Chapisho hilo lilisema kwamba waziri wa uchukuzi nchini humo Katumba Wamala atatoa taarifa ya kina kuelezea namna ya kusonga mbele na matumizi ya mfumo huo.
Waendeshaji magari wamehimizwa waendelee kuwa waangalifu, wamakinike barabarani na kufuata sheria za trafiki.
Mfumo huo almaarufu Electronic Penalty System – EPS unatumia kamera zilizo na uwezo wa kunakili nambari za usajili za magari na makosa yanayofanywa na madereva kama vile kuzidisha kiwango cha kasi.
Madereva wengine walikuwa wameanza kutafuta mbinu za kuzikwepa kamera hizo kama vile kwa kubebea samaki katika sehemu ambazo nambari za usajili za gari zipo.
Tangu matumizi yake yaanzishwe wengi wametozwa faini kwa kuendesha magari kwa kasi ya juu, kutofuata taa za barabarani na makosa mengine.
Faini zilizokuwa zikitozwa ni kati ya shilingi elfu 20 na 200 pesa za Uganda na wakosaji wanastahili kuzilipa katika muda wa siku 28.
Wanaochelewa kulipa wanatozwa faini nyingine ya nusu ya kiwango walichostahili kulipa.