Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), imemfungulia mashtaka aliyekuwa mfanyakazi wa kampuni ya Maji na Majitaka ya Nairobi (NCWSC) Asembo Babra Gladys, kwa madai ya kughushi cheti cha kidato cha nne (KCSE) kupata ajira.
Kulingana na EACC, Asembo alipokea shilingi 6,236,053.10 fedha za umma kwa njia ya ulaghai.
Asembo alifikishwa katika mahakama ya kukabiliana na ufisadi ya Milimani, ambapo alifunguliwa mashtaka kadhaa, ikiwa ni pamoja na kupokea fedha za umma kwa njia ya ulaghai kutoka kampuni ya NCWSC, kutoa habari za uwongo kwa hakimu, kughushi na kuwasilisha cheti bandia.
Tume hiyo ilianzisha uchunguzi baada ya kupokea ripoti kwamba mshukiwa huyo alitumia cheti bandia kupata ajira kama mtaalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwenye kampuni hiyo.
Aidha, uchunguzi huo ulibainisha kuwa cheti alichowasilisha kiliwa bandia, lakini alisingizia kuwa alikipokea kutoka kwa Baraza la Kitaifa la Mitihani Nchini (KNEC).
Mshukiwa huyo alikuwa amekamatwa awali lakini akaachiliwa kwa dhamana ya shilingi 25,000, lakini akaenda mafichoni.
Alikamatwa tena na kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni moja na mdhamini wa kiasi sawa na hicho.