Mercy Johnson aelezea kupungua kwa uzani wa mwili wake

Mashabiki zake mitandaoni na waigizaji wenza walijawa hofu baada ya kuona umbo lake jipya.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwigizaji wa filamu nchini Nigeria Mercy Johnson Okojie ameelezea kilichosababisha apunguze uzani wa mwili kwa kiwango kikubwa katika muda mfupi.

Katika mazungumzo yake na mwigizaji mkongwe Joke Silva, Mercy alielezea kwamba alikumbwa na tishio la saratani akalazimika kufanyiwa upasuaji wa kuondoa tezi.

Kulingana naye, tishio hilo lilijiri wakati mtoto wake wa mwisho alikuwa na umri wa miezi sita pekee na yeye na mume wake wakalazimika kuchukua hatua hiyo.

Hivi maajuzi msanii huyo alichapisha picha zake kwenye akaunti yake ya Instagram ambapo alionekana mdogo kuliko kawaida huku wafuasi wake na waigizaji wenza wakishangaa kilichomfika.

Ilidhaniwa kwamba msanii huyo ambaye huwa anauza bidhaa za kusaidia kupunguza uzani wa mwili alikuwa anaugua au alitumia bidhaa hizo kupita kiasi kwa lengo la kupata mauzo zaidi.

Johnson alielezea pia kwamba kando na upasuaji, madaktari walimpa dawa ambazo huwa anatumia kila siku bila kukosa na sehemu ya madhara ya dawa hizo ni kupungua kwa uzani wa mwili.

Share This Article