Mke wa Rais wa Marekani Donald Trump, Melania Trump ndiye mtu maarufu wa hivi punde zaidi kujiunga na tasnia ya filamu nchini Marekani inayorejelewa na wengi kama Hollywood.
Melania alitoa taarifa hizo kupitia akaunti yake rasmi ya mtandao wa kijamii wa X ambapo aliandika, ” Ninawaletea: MUSE FILMS. Kampuni yangu mpya ya kuandaa filamu.”
Tangazo lake liliambatana na video fupi ya kutangaza filamu ya matukio halisi kuhusu maisha yake ambayo inaangazia siku chache kabla yao kurejea ikulu kwa mara ya pili.
Kulingana naye, kazi hiyo ya sanaa itaonyeshwa kwenye kumbi za filamu kote ulimwenguni kuanzia Januari 30, 2026.
Mwelekezi Brett Ratner ataongoza filamu hiyo ya matukio halisi, ambayo itawapa watazamaji mwonekano wa kipekee wa maisha ya Melania katika wiki za kuelekea kuapishwa kwa mumewe kama rais mwaka 2025.
Filamu hiyo inamfuatilia Melania anapojiandaa kurejea katika maisha ya umma kwa mara ya pili akiwa na familia yake, huku akikabiliana na sarakasi za kila siku.
Bila shaka, Donald ataonekana mara kadhaa pamoja na mwana wao, Barron.