Mcheshi Mzee Majuto akumbukwa Tanzania

Majuto aliyeaga dunia Agosti 8, 2018 akiwa na umri wa miaka 70 alikuwa mchekeshaji na mwigizaji maarufu nchini Tanzania.

Marion Bosire
2 Min Read

Marehemu Alhaji Amri Athumani ambaye alifahamika sana kama Mzee majuto au King Majuto alikumbukwa jana wakati wa hafla ya kutoa tuzo za wachekeshaji nchini Tanzania.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliongoza hafla hiyo na alishiriki moja kwa moja hatua ya kukabidhi washindi fulani tuzo zao katika ukumbi wa Super Dome huko Masaki jijini Dar es Salaam.

Majuto aliyeaga dunia Agosti 8, 2018 akiwa na umri wa miaka 70 alikuwa mchekeshaji na mwigizaji maarufu nchini Tanzania.

Rais Samia alitoa tuzo ya heshima kwa familia ya Mzee Majuto ambayo aliambatanisha na hundi ya shilingi milioni 30 za Tanzania sawa na milioni 1.5 za Kenya.

Majuto anaripotiwa kuanza kuigiza akiwa na umri wa kati ya miaka 9 na 10, wakati huo akihusika kwenye maigizo ya jukwaani moja kwa moja.

Aliwahi kuhusika kwenye maigizo kadhaa ya runinga nchini Tanzania pamoja na filamu kama ile ya “Siri ya Marehemu”.

Wachekeshaji wengine waliotuzwa kwenye usiku huo wa tuzo za ucheshi hafla iliyopatiwa mada ya ‘Cheka na Samia’ ni pamoja na Conrad Kennedy maarufu kama Coy Mzungu.

Coy alinyakua tuzo ambayo haikushindaniwa ya mtu aliyeleta mabadiliko makubwa katika tasnia ya ucheshi nchini humo ambapo pia alituzwa shilingi milioni 10 za Tanzania.

Alikabidhiwa tuzo hiyo na katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na michezo ambaye pia ni msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa.

Msigwa alimpongeza Coy kwa kuwa mchango mkubwa kwa vijana wenye vipaji vya ucheshi nchini Tanzania ambao sasa wamejiunga na tasnia hiyo.

Coy ndiye mwanzilishi wa hafla ya kila mara ya uchekeshaji ya “Cheka Tu”.

Share This Article