Mchekeshaji maarufu wa Uganda Patrick Salvado anaripotiwa kulazwa hospitalini kutokana na matatizo ya kongosho, ugonjwa sawa na ule unaomsibu mwanamuziki nyota wa Uganda Jose Chameleone.
Salvador alichapisha taarifa kuhusu hali yake kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii akisema ugonjwa huo humsumbua mara kwa mara.
“Mara nyingine tena … maumivu haya ni makali mno .. lakini nakubali lawama kwa kukubalia hili kutokea tena. Ninafaa kuwa na ufahamu bora.” Aliandika Salvado.
Salvado anaripotiwa kulazwa katika hospitali ya Nakasero jijini Kampala.
Ugonjwa unaomsibu ni kuharibika kwa kongosho kiungo muhimu kilicho nyuma ya tumbo ambacho huzalisha vimeng’enya muhimu vya chakula kama ‘insulin’.
Kiungo hicho kinapodhurika, vimeng’enya ambavyo kinazalisha huanza kukishambulia hali inayosababisha maumivu makali kwenye tumbo ya juu.
Mitindo ya maisha hulaumiwa kwa kiwango kikubwa kwa kusababisha ugonjwa wa kongosho, ugonjwa ambao hauna tiba, ila ni usimamizi tu wa kuondolea kongosho kazi nyingi.
Jose Chameleone alilazwa hospitalini nchini Uganda mwisho wa mwaka jana kabla ya kuhamishiwa Marekani ambapo alifanyiwa upasuaji wa kuondoa sehemu zilizoharibika za kongosho.
Kwa sasa msanii huyo anatumia dawa ambayo alisema ni ghali mno na iwapo ataikosa basi maisha yake yatakuwa hatarini.
Alirejea nchini Uganda ambapo amekuwa akiendeleza kazi zake kama mwanamuziki.