Algeria watashuka uwanjani Nelson Mandela Namboole mjini Kampala, Uganda, kupambana na Afrika Kusini maarufu kama Bafana Bafana,kuanzia saa kumi na moja jioni katika mechi ya pili ya kombe la CHAN.
Algeria, maarufu kama Desert Foxes, watahitaji ushindi ili kujihakikishia nafasi katika hatua ya nane bora, baada ya kuwacharaza wenyeji Uganda katika mechi ya ufunguzi ya kundi C mabao 3-0.
Bafana Bafana ya Afrika Kusini, ambayo iliwasili Kampala mapema wiki hii, itapania kuanza vyema kwa kuepuka kushindwa.

Timu hizo mbili zitakutana kwa mara ya tano, Algeria ikijivunia kushinda mechi 1 na nyingine tatu kumalizikia sare.
Baadaye saa mbili usiku wenyeji Uganda watakuwa na kibarua dhidi ya Syli National ya Guinea.