Mbunge wa zamani Dalmas Otieno afariki

Marion Bosire
1 Min Read

Mbunge wa zamani wa eneo la Rongo Dalmas Otieno amefariki. Mwanawe Dalmas kwa jina Eddie Otieno, alithibitisha taarifa hizo akielezea kwamba babake aliaga leo asubuhi nyumbani kwake katika mtaa wa Kileleshwa, kaunti ya Nairobi.

Hata hivyo Eddie hakutoa maelezo zaidi kuhusu kilichosababisha kifo cha babake ambaye pia aliwahi kuhudumu kama waziri.

Otieno alichaguliwa kwa mara ya kwanza kabisa kama mbunge wa Rongo mwaka 1988 na kuhudumu kama waziri wa viwanda kati ya mwaka 1988 na 1991.

Mwaka huo wa 1991 alihamishiwa wizara ya Leba na maendeleo ya nguvukazi kabla ya kuelekea katika wizara ya uchukuzi na mawasiliano.

Mwaka 2007 Dalmas Otieno alijiunga na chama cha ODM na kuchaguliwa tena kama mbunge wa Rongo na akachaguliwa kuhudumu kama waziri wa utumishi wa umma katika iliyokuwa serikali ya muungano.

2013 alichaguliwa tena kuongoza watu wa Rongo lakini ilipofika 2017 akashindwa baada ya kujiondoa ODM na kuingia kwenye uchaguzi kama mwaniaji huru.

Safari yake katika huduma serikalini haikuishia hapo kwani mwaka 2018 alichaguliwa kama naibu mwenyekiti wa tume ya mishahara na marupurupu ambako alihudumu hadi mwaka jana.

Share This Article