Mbunge wa eneo la Juja George Koimburi alipatikana leo alfajiri akiwa ametuwa katika shamba la kahawa lililo katika eneo la Kibichoi, kaunti ya Kiambu.
Taarifa za ndani kuhusu kisa cha kupotea kwake na kupatikana hazijawekwa wazi na wahusika hawajatambuliwa.
Koimburi anaripotiwa kufahamisha maafisa wa polisi kwamba alitekwa nyara na kupigwa na watu wasiojulikana waliomchukua nje ya kanisa moja huko Kiambu Jumapili alasiri.
Polisi wamekanusha kuhusika katika kisa hicho lakini wakathibitisha kwamba uchunguzi unaendelea kufuatia ripoti iliyowasilishwa na familia ya mbunge huyo jana Jumapili.
Alipopatikana, Koimburi alikuwa amepoteza fahamu na alikuwa bado amevaa yale yale mavazi aliyokuwa amevaa jana alipotwaliwa na watu hao.
Walioshuhudia walisema kwamba alibebwa kutoka shambani humo na Ambulensi na kupelekwa hospitalini.
Jana mke wa kiongozi huyo kwa jina Ann Koimburi, alisema kwamba mumewe alikabiliwa na wanaume wawili waliojisingizia kuwa waumini ambao walimshika na kumwingiza kwenye gari.
Gari hilo kulingana naye lilikuwa la rangi ya kijivu aina ya Subaru Forester na nambari yake ya usajili kulingana na Anne ilikuwa imeathiriwa kwa lengo la kutatiza utambuzi.
Wanaume hao ambao walikuwa wamevaa mavazi ya raia hawakujitambulisha wakati wa kumchukua Koimburi.