Hazina ya k¥Kitaifa ya Maeneo Bunge ya eneo la Lafey imefadhili kwa asilimia mia moja wanafunzi 150 wa kozi za ualimu kutoka eneo bunge hilo.
Hatua hii ni juhudi madhubuti ya kushughulikia uhaba mkubwa wa walimu katika shule za eneo hilo.
Mbunge wa Lafey, Mohamed Abdi Kheir, alisema kuwa mpango huo wa ufadhili umeundwa ili kusaidia wanaotamani kusomea ualimu, ili baadaye warejee na kufundisha katika shule za eneo hilo.
“Ualimu ni msingi wa kujenga maisha yenye mafanikio. Wanafunzi hawa wa ualimu hivi karibuni wataanza safari yao kama mawakala wa mabadiliko chanya katika eneo letu na hata zaidi” alisema mbunge huyo.
Akizungumza na wanafunzi wa Chuo cha Mafunzo ya Walimu cha Mandera -MTTC, mbunge huyo alihimiza wanafunzi zaidi kufikiria kuingilia ualimu kama taaluma, akisema ni njia muhimu ya kutatua tatizo la uhaba wa walimu kaskazini mwa Kenya.
Mpango huu tayari umewezesha vijana wengi kujiunga na vyuo vya ualimu, na baadhi yao wanatarajiwa kuhitimu hivi karibuni. Kwa sasa, zaidi ya wanafunzi 1,300 wanaendelea na masomo ya ualimu katika MTTC.
Mbunge huyo alisisitiza kuwa serikali yake itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya elimu, rasilimali za kujifunzia na usaidizi kwa walimu ili kuhakikisha kila mtoto katika Lafey anapata elimu bora.
Mkurugenzi wa Elimu wa kaunti ya Mandera, Abdi Sheikh, alisifia mpango huo na kuwahimiza viongozi wengine kuiga mfano huo.
“Elimu ni haki ya kila mtoto. Tunatoa wito kwa viongozi wa maeneo mbalimbali kuwekeza kikamilifu katika elimu ili kulinda mustakabali wa watoto wetu,” alisema Sheikh.
Viongozi wengine wa eneo hilo pia waliwahimiza waliohitimu kidato cha nne kuchangamkia fursa ya kujiunga na vyuo vya ualimu ili kuhakikisha kuwa eneo la kaskazini halikumbwi tena na uhaba wa walimu.