Mbosso kuachia kazi zake za kwanza kama msanii huru Alhamisi

Nyimbo zilizo kwenye EP atakayozindua ndizo za kwanza tangu aondoke WCB

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Tanzania Mbwana Yusuf Kilungi maarufu kama Mbosso ametangaza ujio wa kazi zake za kwanza za muziki akiwa msanii huru, miezi kadhaa baada ya kuondoka WCB.

Mbosso ametangaza kwamba ataachia EP yake mpya aliyoipa jina la ‘Room Number 3’  Alhamisi Juni 12, 2025 kazi aliyoandaa chini ya kampuni yake ya muziki iitwayo Khan Music.

Msanii huyo alifuta machapisho yake ya awali akiwa WCB kutoka kwenye akaunti yake ya Instagram na kubakisha yanayohusu EP ambayo atazindua Room Number 3 kwa kifupi RN3.

Kuna video moja fupi ambayo amechapisha inayokaribisha mashabiki wake ‘Nyumbani’ kisha mtoto mdogo anaonekana akisoma wasifu wake ambao unaanza na tarehe ya kuzaliwa ya Mbosso, Oktoba 3, 1995.

Kulingana na maelezo kwenye video hiyo Room Number 1 ni wakati alianza kazi kama mwanamuziki akiwa na umri wa miaka 18 wakati huo akiwa kwenye bendi ya Yamoto.

Room Number 2 huenda ikawa wakati ambapo alisajiliwa na kampuni ya mwanamuziki mwenza Diamond Platnumz ya WCB alikokaa kati ya mwaka 2018 na mwaka huu wa 2025.

Inaaminika kwamba Room Number 3 sasa ni Mbosso chini ya usimamizi wake binafsi kama mwanamuziki.

Kulingana na video na picha alizochapisha, kazi hiyo huenda imeandaliwa kijijini ambako amekaa kwa muda tangu alipoondoka WCB yapata miezi minne iliyopita.

Kuonekana kwake kijijini muda mrefu kulisababisha minong’ono mitandaoni wengi wakidhania kwamba alifilisika akashindwa kumudu maisha mjini akarejea nyumbani.

Alikanusha dhana hiyo kwenye mahojiano na kuahidi mashabiki wake kazi mpya.

Share This Article