Waziri wa Fedha John Mbadi sasa anasema kauli zake juu ya ufadhili wa elimu ya bure katika shule za umma zilinukuliwa vibaya.
Hata hivyo, Mbadi alikataa kufafanua alichomaanisha wakati alipokutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) Abdi Mohammud na Mwenyekiti wa tume hiyo Dkt. David Oginde leo Jumatano.
Mbadi amekumbana na shutuma kutokana na kauli alizotoa bungeni kwamba serikali haina fedha za kutosha kufadhili kikamilifu elimu ya msingi bila malipo.
Aliyasema hayo Alhamisi wiki iliyopita alipofika mbele ya Kamati ya Bunge la Taifa juu ya Elimu kujibu maswali kuhusiana na sekta ya elimu nchini.
Kauli hizo zilishutumiwa vikali na wadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja na chama cha KUDHEIHA, walioonya kuwa hatua hiyo itawanyima wanafunzi wengi kutoka familia maskini haki ya kupata elimu ikiwa itachukuliwa.
“Mambo ya Free Basic Education, hatumwombi mtu yeyote. Tunasema ni lazima mpango huo uendelee,” alifoka mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro.
“Hatutakubali yeyote kufanya mchezo na suala la elimu ya msingi bila malipo. Chumi hujengwa na watu, kazi ya elimu ni kuongeza thamani kwa watu, kwa wafanyakazi katika mantiki ya kiuchumi. Elimu huongeza thamani kwa wafanyakazi ambao ni watu, na uchumi wa Kenya unaweza kukua tu ikiwa elimu itapatikana kwa wote, ni elimu bora na kila mtu ako na fursa ya kuipata.”
Shutuma zilizoilazimu serikali ya Kenya Kwanza kujitokeza na kufutilia mbali hofu kuwa ufadhili wa elimu ya bure nchini utaondolewa.
Katibu wa Idara ya Elimu ya Msingi Prof. Julius Bitok hata hivyo alilitaka bunge kuongeza mgao wa fedha kwa Wizara ya Elimu ili kuwezesha ufadhili wa elimu katika shule za umma.