Rais William Ruto jana Jumanne jioni aliongoza mkutano wa wapatinishi wa kuleta amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Wapatanishi hao walichaguliwa chini ya mchakato wa amani wa pamoja wa Luanda na Nairobi, uliojukumiwa kutafuta suluhu ya kudumu kwa mzozo Mashariki mwa DRC. Mkutano huo uliandaliwa kwa njia ya video.
Wapatanishi hao wanajumuisha Marais wastaafu Uhuru Kenyatta (Kenya) Olusegun Obasanjo (Nigeria), Sahle-Work Zewde (Ethiopia) na Catherine Samba-Panza wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na ile ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), zimeandaa mikutano ya pamoja jijini Dar es Salaam, Tanzania na kupitia njia ya mtandaoni, kwa lengo la kukomesha machafuko yanayoghubika Mashariki mwa DRC.
Aidha, maafisa wa vikosi vya usalama wa jumuiya hizo mbili, pia wameshiriki mazungumzo ya pamoja ili kubuni mikakati itakayotumika katika kukomesha ghasia nchini DRC.
Eneo la Mashariki mwa DRC linazidi kukabiliwa na ukosefu wa usalama huku vikosi vya serikali vikikabiliana na wapiganaji wa M23 ambao hadi kufikia sasa wametwaa mji wa Goma ambao ndio wa pili kwa ukubwa nchini humo.