Tume ya Kitaifa ya Mshikamano na Utangamano (NCIC), kwa ushirikiano na Shirika la Utangazaji Nchini (KBC), imezindua misururu ya mazungumzo baina ya vizazi katika kaunti ya Marsabit.
Mazungumzo hayo yanalenga kuziba pengo lililopo baina ya vizazi tofauti kupitia mijadala iliyo wazi.
Akizungumza kabla ya uzinduzi huo chini ya kauli mbiu #AmaniKwaGround, Naibu Mkurugenzi wa NCIC kuhusu amani na maridhiano Liban Guyo, alisisitiza haja ya kuwahusisha wakenya wote katika majadiliano yanayohusu changamoto kuu zinazoghubika taifa hili.
“Tuko katika kaunti ya Marsabit kuzindua mazungumzo ya kitaifa kwa ushirikiano na KBC. kuanzia saa moja jioni hadi saa tatu usiku, tutajadili maswala kuhusu uongozi kutoka kbla ya taifa hili kupata uhuru hadi wakati wa kizazi cha Gen X, Millennials na Gen Z.” alisema Guyo.

Kulingana na Guyo, mazungumzo hayo ni sehemu ya juhudi za kutoa jukwaa ambapo watu wote watasikika, hususan vijana watapata fursa ya kujieleza na kujumuishwa katika mipango ya kuboresha taifa hili.
“Tuligundua kwamba vizazi tofauti nchini Kenya havizungumzi baina yavyo. Sio tu pengo la vizazi, lakini pia pengo katika kusikiliza,” alidokeza Guyo.
Kwa upande wake, David Saruni, Naibu Kamishna wa Kaunti ya Marsabit ya Kati alielezea umuhimu wa kipekee wa kuandaa mazungumzo ya kwanza katika kaunti hiyo, ikizingatiwa kuwa kaunti hiyo inakabiliwa na mizozo ya kijamii.