Katika mkutano wa baraza la mawaziri uliofanyika leo Jumanne Machi 11, 2025, Rais William Ruto na kundi lake waliidhinisha mabadiliko yanayolenga kuimarisha vyama vya ushirika.
Mabadiliko hayo yanalenga kuhakikisha udhabiti, ufanisi na uwezo wa ushindani wa vyama hivyo vya kuweka akiba na kutoa mikopo kote nchini.
Mabadiliko yaliyopendekezwa yaliyo kwenye mswada wa vyama vya ushirika vya akiba na mikopo wa mwaka 2023, yanaangazia kufanya shughuli za kifedha na za kiteknolojia za vyama hivyo kuwa za kisasa.
Mojawapo ya vipengele vikuu ni kuanzisha mfumo wa pamoja wa huduma za vyama hivyo, utakaoviwezesha kukusanya mapato, kupitisha suluhisho za usimamizi wa kiteknolojia wa masuala ya kifedha na kushirikiana kwa njia bora.
Kituo cha pamoja cha ukwasi pia kitaanzishwa ili kuwezesha miamala kati ya vyama mbali mbali, ukopeshaji wa muda mfupi na uhusika katika mpango wa kitaifa wa malipo.
Baraza la mawaziri limeunga mkono pia mabadiliko katika hazina ya udhamini wa michango ya wanachama ili kutoa ulinzi bora kwa michango ya wanachama, kupunguza hatari ya dhamana ya serikali na kuimarisha sekta ya ushirika wa kifedha.
Mabadiliko hayo yanatarajiwa kupunguza gharama ya shughuli za vyama hivyo, kuimarisha uvumbuzi na kuimarisha imani ya umma katika vyama hivyo kwa kuviweka kuwa wahusika muhimu katika juhudi za Kenya za ujumuishaji wa kifedha na uwezeshaji wa kiuchumi.
Haya yanajiri siku kadhaa baada ya ripoti kuibuka kwamba shilingi bilioni 6 ziliondolewa kwa njia isiyofaa kwenye akaunti ya muungano mkuu wa vyama vya ushirika nchini – KUSCCO na hivyo kusababishia vyama hivyo hasara.