Mawakili wa Diddy wataka hukumu sawa na muda aliozuiliwa

Marion Bosire
2 Min Read
P Diddy

Mawakili wa mwanamuziki aliyezuiliwa Sean “Diddy” Combs wanasema kwamba anastahili kuhukumiwa kifungo cha gerezani kinacholingana na muda ambao amekaa kizuizini.

Katika ombi walilowasilisha mahakamani Jumanne, mawakili hao wanasema wanahisi kwamba Combs anastahili kifungo kisichozidi miezi 14 ambayo amekaa kizuizini.

Haya yanafuatia hatua ya jopo la waamuzi wa kesi yake ya kumpata na hatia mapema mwaka huu ya kusafirisha watu kwa ajili ya kuwatumia kwa biashara ya ngono.

Mawakili hao wanahisi muda umefika wa Combs kurejea nyumbani kwa familia yake wakisema sheria ya Mann hutumika dhidi ya watu wanaoendesha mtandao wa ngono na mteja wao hakufanya hivyo.

Wanasema pia kwamba Diddy hakuwahi kufanya ngono na makahaba wa kiume wala hakuhusika moja kwa moja katika kupanga usafirishaji wao kuvuka mipaka ya majimbo.

Mawakili wake wanasema kwamba Diddy alikuwa tu mtazamaji na mpiga picha wa ngono wa kujitegemea ambaye alipenda kurekodi video za wapenzi wake wa zamani wakifanya ngono.

Hata hivyo, waendesha mashtaka wa serikali wamepinga madai hayo wakisema kulikuwa na ushahidi wa kutosha kuunga mkono hukumu za jopo la waamuzi chini ya Sheria ya Mann.

Kulingana nao, Diddy ndiye alikuwa mbunifu mkuu wa kila kipengele cha sherehe zake chafu maarufu.

Maafisa wa serikali pia wamepinga dhana kwamba Diddy alipenda tu kutazama, wakisema alishiriki kikamilifu kwa kuelekeza mienendo ya kingono kati ya makahaba na waathiriwa na akijichua wakati wote wa matukio hayo ya kingono.

Zaidi ya hayo, waendesha mashtaka walidai kwamba hoja ya Diddy kuwa yeye alikuwa kama mtayarishaji wa filamu za ngono anayelindwa chini ya Marekebisho ya Kwanza ya Katiba haina mashiko.

Sababu wanayotoa ni kwamba nyingi ya sherehe hizo hazikurekodiwa na kwa zile zilizorekodiwa, mara nyingi Diddy hakutoa taarifa mapema kuwa atakuwa akirekodi, na washiriki wengi hawakutoa ridhaa yao kwa kurekodiwa.

Share This Article