Hatima ya konstebo wa polisi Klinzy Barasa Masinde sasa i mikononi mwa mahakama.
Hii ni baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga kuidhinisha mashtaka ya mauaji dhidi yake.
Masinde anatuhumiwa kwa kumfyatulia risasi mchuuzi wa barakoa Boniface Kariuki kwenye maandamano ya kulalamikia kuuawa kwa mwanablogu na mwalimu Albert Ojwang Juni 17, hatua iliyosababisha kifo cha mchuuzi huyo wakati akipokea matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kenyatta.
Masinde alifika mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Milimani Kanyi Kimondo leo Alhamisi ili kujibu mashtaka dhidi yake.
Jaji Kimondo aliagiza kuwa Masinde azuiliwe katika gereza la Nairobi na kufanyiwa uchunguzi wa akili kabla ya kujibu mashtaka dhidi yake.
Mshukiwa anatarajiwa kufikishwa tena mahakamani Julai 28 mwaka huu.