Mauaji ya mchuuzi Boniface Kariuki: Afisa mmoja wa polisi yuko huru

Hata hivyo, Konstebo Klinzy Masinde Barasa anakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya mchuuzi wa barakoa, Boniface Kariuki kwenye maandamano ya Juni 25.

Martin Mwanje
1 Min Read
Konstebo Klinzy Masinde Barasa anayekabiliwa na mashtaka ya mauaji

Ni afueni kwa Konstebo Duncan Kiprono, afisa wa polisi ambaye ni mshukiwa wa pili aliyekuwa akikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya mchuuzi wa barakoa Boniface Kariuki mwenye umri wa miaka 22. 

Hii ni baada ya mahakama ya Milimani kupuuzilia mbali ombi la kuendelea kumzuilia kuhusiana na mauaji hayo kutokana na kukosekana kwa sababu za kufanya hivyo.

Kwa upande mwingine, Hakimu anayesikiliza kesi hiyo Benmark Ekhubi ameridhia mshukiwa wa kwanza Konstebo Klinzy Masinde Barasa kukiri mashtaka ya mauaji yanayomkabili.

Masinde alinakiliwa kwenye video akimfyatulia risasi Kariuki wakati wa maandamano ya Juni 25 yaliyoitishwa na vijana wa Gen Z jijini Nairobi.

Afisa huyo wa polisi anatarajiwa kukiri mashtaka dhidi yake Julai 28, 2025.

Hii ni baada ya Ofisi ya Kiongozi wa Mashtaka ikiongozwa na wakili Vincent Monda, kuomba muda zaidi ili mshukiwa afanyiwe tathmini ya akili miongoni mwa mambo mengine.

Kisa cha Kariuki kufyatuliwa risasi iliyomsababishia mauti kimeibua shutuma dhidi ya maafisa wa polisi wanaotuhumiwa kwa kuwakandamiza waandamanaji wakati wa maandamano ya Juni 25 na ya Saba Saba ambapo makumi ya waandamanaji waliuawa na wengine kujeruhiwa.

Ibada ya kumbukumbu ya Kariuki iliandaliwa jana Jumatano wakati mipango ya mazishi ikiendelea.

 

 

 

 

Share This Article