Master J azua maoni tofauti ya wanamuziki

Mtayarishaji huyo wa muziki alisema wasanii wa Tanzania hawawezi kuimba jukwaani moja kwa moja.

Marion Bosire
2 Min Read

Mtayarishi wa muziki nchini Tanzania Joachim Marunda Kimaryo, maarufu kama Master J ambaye ni muandaaji wa muziki nchini Tanzania amezua maoni tofauti kuhusu muziki nchini Tanzania.

Jaji huyo wa shindano la kutafuta vipaji vya muziki nchini Tanzania la Bongo Star Search alitoa maoni yake kuhusu tamasha la tuzo za Trace lililoandaliwa maajuzi Zanzibar, nchini Tanzania.

Mzoefu huyo wa muziki alisema kwamba wasanii wa muziki nchini Tanzania hawana uwezo wa kutumbuiza jukwaani moja kwa moja bila kuchezewa muziki wao uliorekodiwa.

Kulingana naye iwapo wasanii tajika wa Tanzania wangewekwa pamoja kwenye tamasha moja wapambane na msanii Bien Barasa wa kenya, basi Bien angewashinda kwa kiwango kikubwa.

Wasanii wengi wa Tanzania walionekana kulemewa na uimbaji wa moja kwa moja wakitumia bendi jukwaani wakati wa tuzo za Trace huku Bien akionyesha weledi wake katika hilo.

Msanii Marioo wa Tanzania alipokuwa akiimba wimbo aliomshirikisha Bien alilemewa na sauti na maneno ya wimbo huo hadi pale ambapo Bien aliingia jukwaani na kumsaidia.

Wapo wasanii ambao wamechukulia vizuri ukosoaji wa Master Jay na wapo wengine ambao wamechukizwa na maoni yake.

Juma Jux ambaye alishinda tuzo ya msanii bora wa tanzania kwenye tuzo hizo za Trace alisema haya kuhusu maoni ya Jay, “Maoni yake ninayaheshimu, ninaamini kile anachokisema kina maana ndani yake.”

Jux aliendelea kusema kwamba kuna vitu ambavyo wanafaa kujifunza kama wasanii kutoka kwa usemi wa mtayarishaji huyo wa muziki.

Diamond naye alisema kwamba atatumia maneno ya Master Jay kujirekebisha kama msanii.

Lakini Ali Kiba ambaye hakupata fursa ya kutumbuiza kwenye tuzo za Trace anaonekana kuchukizwa na usemi wa Master Jay.
Jay alimtaja Ali Kiba kama mmoja wa wasanii ambao hawawezi kutumbuiza moja kwa moja bila rekodi kwani huwa anabana pua.

Kiba alimjibu akisema Master Jay amekuwa akiropokwa bila kujiheshimu asijue yeye ni nani. Alishangaa iwapo yeye ndiye wa kupandisha watu hadhi maishani.

Share This Article