Mkuu wa utumishi wa umma Felix Koskei, ameagiza mashirika yote ya serikali kuanza kutoa huduma za manunuzi kupitia mfumo wa kielektroniki wa serikali almaarufu e-GP mara moja.
Koskei amesema agizo hilo linafaa kutekelezwa kikamilifu bila kuchelewa, akisema ndiyo njia pekee ya kuhakikisha uwazi na kujenga imani ya umma.
Akiongea siku ya Ijumaa alipohutubia mkutano wa viongozi wakuu serikalini katika kaunti ya Mombasa, Koskei alisema hatua hiyo itasaidia kuepusha ufisadi ambao umewanyima wananchi fursa ya kunufaika na huduma za serikali.
“Tusiwe na sababu au juhudi zozote za kutekeleza agizo hili. Mfumo huu lazima ufanye kazi na lazima ukumbatiwe katika taasisi zote za umaa,” alisema Koskei.
Koskei pia aliwataka wasimamizi wa mashirika ya serikali kuzingatia uadilifu na nidhamu katika utekelezaji wa majukumu yao, na kuhakikisha kwamba mashirika hayo ya umma yanahudumu ipasavyo, ili kufanikisha malengo ya serikali.
Mkutano huo unawaleta pamoja makatibu wa wizara, wakuu wa mashirika ya serikali na asasi nyingine za usimamizi, ili kushughulikia masuala muhimu katika utumishi wa umma.