Mashirika mbalimbali yashinikiza kuachiliwa kwa Besigye, wengineo

Martin Mwanje
2 Min Read
Wawakilishi wa mashirika mbalimbali wakiwahutubia wanahabari siku ya Jumanne

Jumla ya mashirika 12, yakiwemo ya kutetea haki za binadamu na kitaaluma, yametoa wito kwa mamlaka za Uganda kumwachilia huru mara moja kiongozi wa upinzani nchini humo Dkt. Kizza Besigye. 

Mashirika hayo pia yanashinikiza kuachiliwa kwa Hajj Obeid Lutale, Eron Kiiza na wengine wote waliokamatwa kinyume cha sheria.

“Siku 18 zimepita tangu Mahakama ya Juu ya Uganda ilipotoa uamuzi Januari 31, 2025 kwamba kushtakiwa kwa raia katika mahakama za kijeshi katika kesi za jinai ni kunyume cha katiba na kwamba kesi yoyote ya aina hiyo ihamishiwe mahakama za kawaida,” walisema wawakilishi wa mashirika hayo wakati wakiwahutubia wanahabari jijini Nairobi.

“Licha ya uamuzi wa Mahakama ya Juu na maombi ya kisheria ya kutaka Kizza Besigye, Hajj Obeid Lutale, mwanasheria Eron Kiiza na wengineo kuachiliwa huru, mamlaka za Uganda zimepuuza maagizo ya mahakama na kuendelea kuwanyima uhuru wao bila mantiki.”

Afya ya Dkt. Besigye imezorota katika kipindi cha karibu wiki mmoja iliyopita baada ya kiongozi huyo ambaye ameumezea mate wadhifa urais mara kadhaa kususia chakula.

Ni azima yake hiyo ambayo imemweka matatani na utawala wa Rais Yoweri Museveni.

Uchaguzi mkuu nchini Uganda utaandaliwa mwaka 2026 na haijabainika ikiwa Dkt. Besigye atagombea tena urais.

Dkt. Besigye na Lutale walitekwa nyara na watu wasiojulikana mwaka jana wakati walipokuwa wametembelea Kenya kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa kitabu cha kinara wa chama cha Narc K Martha Karua jijini Nairobi.

Mashirika hayo 12 yakilaani utekaji nyara huo walioutaja kuwa ukiukaji wa sheria ya kimataifa.

Mashirika hayo yanajumuisha Amnesty International, Centre for Strategic Litigation (CSL), IMLU, ICJ – Kenya, KHRC, KMPDU na LSK.

Mengine ni PALU, Mwanzo.org, East Africa Law Society, Vocal Africa na Change Tanzania Movement.

 

 

Share This Article