Maseneta waigeukia EACC, waitaka kuelezea hatua walizochukuliwa Magavana wabadhirifu

Martin Mwanje
1 Min Read
Moses Kajwang - Mwenyekiti wa kamati ya Seneti ya CPAC

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imetakiwa kuelezea hatua ilizochukua dhidi ya serikali za kaunti ambazo zilibainika kubadhiri fedha za umma.

Kamati ya Uhasibu wa Umma ya Bunge la Seneti (CPAC) pia imeitaka EACC kuelezea ilivyoshughulikia masuala mengine husika yaliyoibuliwa na kamati hiyo.

EACC sasa ina miadi na kamati hiyo Septemba 11 mwaka huu.

Ikiongozwa na mwenyekiti wake Moses Kajwang, kamati hiyo inasema mwenyekiti na mkurugenzi mtendaji wa tume hiyo wanapaswa kuwaarifu Maseneta kuhusu hadhi ya kila kaunti na ikiwa kuna uwezekano wamependekeza baadhi ya Magavana kushtakiwa, basi inahitaji ripoti kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kuthibitisha hilo.

Aidha, wameonya Magavana watakaosusia kufika mbele yao kuwajibishwa wakisema watakiona cha mtema kuni ikiwa watafanya hivyo.

Kinyume cha msimamo wa kinara wa chama cha ODM Raila Odinga kwamba ni serikali za kaunti zinazopaswa kuwawajibisha Magavana, Maseneta wanashikilia kuwa ni wajibu waoi kufanya hivyo ili kuangazia matumizi ya fedha za umma.

Hujuma ya Maseneta dhidi ya EACC inawadia wakati ambapo madai yamekithiri kuwa kamati za bunge zimekuwa mstari wa mbele kuitisha mlungula kutoka kwa watu wanaofika mbele yake kuwajibishwa, wakiwemo Magavana.

TAGGED:
Share This Article