Kamati ya Bunge la Seneti kuhusu Fedha na Bajeti ilifanya kikao muhimu na Tume ya Ugavi wa Mapato – CRA kujadili mapendekezo ya kiwango cha juu zaidi kinachokubalika cha matumizi ya kawaida kwa serikali za kaunti kwa mwaka wa kifedha 2026/2027 na miaka inayofuata.
Wajumbe wa kamati walikubaliana kwamba kuanzisha mchakato wa maandalizi ya bajeti mapema kutaboresha upangaji na kuleta matokeo bora zaidi ya kifedha kwa kaunti.
Mwenyekiti wa CRA Mary Wanyonyi Chebukati, aliyeongoza ujumbe wa tume hiyo, alibainisha changamoto kubwa ni kucheleweshwa kunakoendelea au kutowasilishwa kwa takwimu muhimu za kifedha kutoka kwa serikali na mabunge ya kaunti.
Alisema kuwa hali hii inazuia uwezo wa CRA kufanya uchambuzi sahihi na kubuni mifumo ya usawa wa ugavi wa rasilimali.
Majadiliano yalijumuisha mapendekezo ya mageuzi ya kisheria, ambapo maseneta na makamishna wa CRA walichunguza uwezekano wa kurekebisha kanuni ya 25 ya sheria ya usimamizi wa fedha za umma au sheria zingine husika, wakitaja udhaifu katika mfumo wa sasa.
Naibu mwenyekiti wa kamati hiyo Tabitha Mutinda, alisisitiza umuhimu wa kuweka rasmi wajibu wa utoaji takwimu, akisema, “Kuna haja ya mfumo wa pamoja, labda wa kisheria, wa kuhitaji kaunti kutoa takwimu. Hii itahakikisha uwajibikaji na kuboresha ubora wa maamuzi ya bajeti.”
Aidha, alihimiza CRA kushirikiana zaidi na kamati ya fedha kuwasilisha rasimu za mapendekezo na kujadili marekebisho yanayopendekezwa ya sheria hiyo.
Kikao kilihitimishwa kwa pande zote mbili kuthibitisha tena dhamira yao ya kuimarisha ushirikiano ili kusaidia utoaji bora wa huduma katika serikali za kaunti.