Masaka Kids kuangaziwa kwenye Netflix

Marion Bosire
2 Min Read

Kundi la watoto wacheza denzi kutoka nchini Uganda litaangaziwa katika filamu ya matukio halisi itakayowekwa kwenye jukwaa la mitandaoni la Netflix.

Kampuni ya Archewell Productions inayomilikiwa na mwanamfalme Harry na mkewe Meghan Markle inashirikiana na Netflix katika maandalizi ya filamu hiyo kuhusu wacheza densi hao wa umri mdogo.

Watoto hao wa Masaka Kids Africana walijipatia umaarufu sana ulimwenguni wakati wa janga la Covid 19, kufuatia kusambaa kwa kazi zao mitandaoni.

Filamu hiyo imepatiwa jina la “Masaka Kids, A Rhythm Within” inaangazia watoto hao mayatima waliopoteza wazazi wao kufuatia vita, njaa na magonjwa na ambao waligeukiwa densi na muziki kama chanzo cha matumaini.

David Vieira Lopez na Moses Bwayo ndio waelekezi wa kazi hiyo huku waandalizi wakiwa studio za Campfire na kampuni ya maandalizi ya Wontanara pamoja na Harry na Meghan.

Harry na Meghan waligundua kundi hilo wakati wa Corona huku mwanao wa kiume aitwaye Archie akiwapendelea sana ndiposa wakaamua kuandaa kazi hii inayotarajiwa kuzinduliwa baadaye mwaka huu.

Hassan Suuna aliasisi kundi hilo la Masaka Kids mwaka 2013 kama njia ya kusaidia mayatima zaidi ya 200 katika eneo la Masaka.

Densi zao zimegusa watu maarufu ulimwenguni wakiwemo wanamuziki Janet Jackson na Drake na akaunti yao ya YouTube imekua sana na sasa ina wafuatiliaji zaidi ya milioni 4.

Share This Article