Masaibu ya Waititu: Korti yakataa kubatilisha kifungo cha miaka 12

Martin Mwanje
2 Min Read
Ferdinand Waititu - Gavana wa zamani wa Kiambu

Gavana wa zamani wa Kiambu Ferdinand Waititu alipata pigo jana Jumanne baada ya mahakama kukatalia mbali ombi lake la kutaka kubatilisha kifungo cha miaka 12 alichohukumiwa mapema mwaka huu. 

Waititu aliwasilisha ombi hilo Agosti 28 ambapo alitaka hukumu ya miaka 12 dhidi yake kuhusiana na mashtaka ya ufisadi ibatilishwe.

Hii ni baada ya kupatikana na hatia kuhusiana na mashtaka ya ufisadi dhidi yake na kuagizwa kulipa shilingi milioni 53.5 au afungwe miaka 12 jela.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Renson Ingonga alipinga vikali ombi hilo, pingamizi ambayo imezaa matunda hiyo jana baada ya mahakama kukataa ombi hilo.

Katika uamuzi uliotolewa na Jaji Lucy Njuguna, mahakama ilibaini kwamba Waititu alikosa kudumisha kanuni za uongozi bora na kulinda fedha za umma baada ya kupokea kwa njia ya ulaghai shilingi milioni 25 kutoka kwa kampuni ya Testimony Enterprises.

Jaji Njuguna alisema hukumu hiyo itadumishwa hadi rufaa iliyowasilishwa na Waititu kuipinga itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Isistohe, Jaji huyo aliagiza kwamba hukumu hiyo isikilizwe na kuamuliwa ndani ya siku 120, akionya kuwa ikiwa Waititu atachelewesha kusikilizwa kwa rufaa hiyo kwa namna yoyote, basi itatupiliwa mbali.

Wakati huohuo, Gavana huyo wa zamani wa Kiambu, maarufu kama Baba Yao, ataendelea kutumikia kifungo chake katika gereza la Kamiti baada ya kukosa kutimiza masharti ya dhamana yaliyomhitaji kuweka shilingi milioni 53 kwenye benki.

Kesi hiyo itatajwa Oktoba 1, 2025.

 

 

 

Share This Article