Marais wawili wa zamani wa Malawi jana Jumapili walizindua kampeni tofauti za kumng’oa madarakani Rais wa sasa wa nchi hiyo Lazarus Chakwera.
Uchaguzi mkuu nchini humo umepangwa kufanyika Septemba 16 mwaka huu.
Mashaka juu ya mfumko wa bei unaokaribia kufika asilimia 30 na mdororo mkubwa wa kiuchumi vinatarajiwa kutawala kampeni kuelekea uchaguzi katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.
Takriban robo tatu ya watu milioni 21 nchini humo wanaishi kwenye umaskini mkubwa, kwa mujibu wa Benki ya Dunia.
Akiwahutubia maelfu ya wafuasi wake katika mji wa pili kwa ukubwa nchini Malawi wa Blantyre, mpinzani wa muda mrefu wa Chakwera Peter Mutharika, 85, aliapa “kuokoa” nchi hiyo kutoka kwenye changamoto za kiuchumi na kisiasa.
Mutharika, ambaye ni Profesa mstaafu wa sheria, anaongoza chama kikuu cha upinzani cha Democratic Progressive, na alihudumu kama rais kuanzia mwaka 2014 hadi 2020, wakati kuchaguliwa kwake tena kulifutiliwa mbali kwa sababu za udanganyifu.
“Leo, Malawi iko chini ya mateso — njaa, umaskini, na uoga wa serikali inayopaswa kutulinda,” alisema Mutharika.
Viongozi wa upinzani wamekishutumu chama tawala cha Malawi Congress Party cha Chakwera kwa kukandamiza upinzani.
Rais wa zamani Joyce Banda wa chama cha People’s Party, pia alizindua kampeni zake jana Jumapili katika mji wa katikati mwa nchi hiyo wa Ntcheu.
Banda, mwenye umri wa miaka 74, aliahidi kutoa kipaumbele kwa uwezeshaji wa vijana na kubuni nafasi za ajira.
Banda alichukua hatamu za kuiongoa nchi hiyo mnamo mwaka 2012 kufuatia kifo cha Rais Bingu wa Mutharika.
Alikuwa akihudumu kama Naibu Rais wakati huo.