Mandera yaadhimisha siku ya kimataifa ya amani

Marion Bosire
2 Min Read

Dunia ilipokuwa ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Amani, wakazi wa Kaunti ya Mandera walikusanyika kwa pamoja kutoa wito wa mshikamano ili kuimarisha amani ya kudumu katika eneo hilo.

Viongozi wa eneo hilo, wazee na maafisa wa serikali walihudhuria maadhimisho hayo ambapo suala la migogoro ya mara kwa mara ya koo liliibuliwa kama kikwazo kikuu kwa amani na maendeleo endelevu.

Jamii za Mandera zilitakiwa kuweka kando tofauti zao, kukumbatia mazungumzo na kushirikiana kwa karibu na mashirika ya serikali ili kukomesha ghasia za mara kwa mara ambazo zimeathiri maisha na riziki kwa miaka mingi.

Kwa sauti moja, jamii ya Mandera ilithibitisha tena kujitolea kwake kwa juhudi za kujenga amani, ikiahidi kuunga mkono juhudi za maridhiano na kuboresha usalama katika maeneo yaliyoathirika zaidi.

Liban Guyo, amaye ni Naibu Mkurugenzi katika Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa NCIC, alitoa wito wa kuanzishwa kwa mifumo imara ya utatuzi wa migogoro ili kushughulikia mizozo na kuhakikisha wahusika wa machafuko wanawajibishwa.

“Ili amani itawale, hakuna mhalifu anayepaswa kulindwa. Wanaosababisha hali ya kutoaminiana na vurugu lazima waondolewe ili haki itendeke,” alisema Guyo.

Naibu Kamishna wa Kaunti ya Mandera, Solomon Cheboton, alisisitiza umuhimu wa kuanzisha mifumo ya onyo la mapema kuhusu mabadiliko ya tabianchi ili kusaidia jamii kushirikiana katika kutumia rasilimali zilizopo na kupunguza ushindani unaochochea migogoro.

“Ni lazima tuendelee kudumisha amani kila wakati ili maendeleo yaweze kupatikana kote katika Kaunti ya Mandera,” aliongeza Cheboton.

Wadau wa amani katika Mandera pia waliahidi kuendelea kueneza ujumbe wa amani kila kona ya kaunti hiyo, kwa lengo la kujenga Mandera iliyoungana na yenye maelewano.

Share This Article