Nile Crocodiles ya Sudan iliwatema nje Desert Foxes kutoka Algeria na kufuzu kwa nusu fainali ya kipute cha CHAN.
Sudan iliwapiga Algeria penati 4-2, baada ya kutoshana nguvu bao 1-1, ndani ya dakika 120 katika robo fainali ya Jumamosi usiku uwanjani Amaan, Zanzibar.
Sudan walichukua uongozi dakika ya 48 baada ya Ayoub Ghezala wa Algeria kujifunga.
Soufiane Bayazid alikomboa bao hilo dakika saba kabla ya kipenga cha mwisho, na pande zote kufunga milango hadi dakika zote 30 za ziada.
Sudan watafunga safari hadi Dar es Salaam, kwa nusu fainali ya kwanza Jumanne hii dhidi ya Madagascar kuanzia saa kumi na moja unusu.
Baadaye mabingwa mara mbili wa kombe hilo, Simba wa Atlas kutoka Morocco, watavaana na mabingwa watetezi, Simba wa Teranga kutoka Senegal, kuanzia saa mbili unusu.