Mama Taifa Rachel Ruto, ametoa wito wa ushirikiano dhabiti ili kupanua mpango wa lishe shuleni katika shule za umma na kote nchini.
Akizungumza katika shule ya msingi ya Kachororoni, Ganze, kaunti ya Kilifi alipokuwa akiongoza upanuzi wa mpango wa utoaji maziwa shuleni, Mama Taifa alihimiza asasi za serikali, wadau wa sekta ya kibinafsi na jamii kushirikiana kumaliza njaa shuleni.
“Pakiti ya maziwa ni muhimu sana kwa mwanafunzi. Kuwekeza katika lishe ya mwanafunzi, ni kuwekeza kwa mustakabal wa taifa,”alisema Mama Taifa.
Mama Taifa alisema kuwa kuwapa wanafunzi maziwa pamoja na kutekeleza ukuzaji wa mboga na matunda shuleni, hupiga jeki upatikanaji wa lishe bora na utoshelevu wa chakula, hatua inayoimaisha shughuli za masomo.
“Lengo letu la kumaliza njaa, unahusisha kuwezesha shule kupitia uzalishaji wa chakula na kubuni uhusiano wa kujitegemea kati ya elimu na lishe bora,”alidokeza Mama Taifa.
Aliwapongeza wanafunzi 22 wa shule ya msingi ya Kachororoni ambao wamebuni bustani za mashamba nyumbani baada ya kupata ujuzi shuleni.
Mama Taifa alikuwa ameandamana na Naibu Gavana wa Kilifi Flora Chibule, mwakilishi wanawake kaunti ya Kilifi Gertrude Mbeyu, na viongozi wengine wa eneo hilo.