Mama Ida Odinga amesimulia kuhusu jinsi yeye na marehemu mume wake Raila Amolo Odinga walichagua majina ya wanao wanne waliobarikiwa nao katika ndoa yao ya miaka 52.
Akizungumza wakati wa kutoa ujumbe wake wa kumwomboleza Raila katika ibada ya wafu uwanjani Nyayo, Ida alisema kwamba mwanao wa kwanza marehemu Fidel Castro Odhiambo Odinga, alipatiwa jina hilo na marehemu Raila.
Mama Ida anasema alishangaa ni kwa nini mume wake alichagua jina hilo lakini akamwelezea kwamba alikuwa anampenda sana Fidel Castro kiongozi wa zamani wa Cuba.
Walipojaliwa mwanao wa pili wa kike, Ida na Raila walimpa jina Rosemay, Rose ni jina la mama mzazi wa Ida na Mary ni jina la mamake Raila.
Mwanao wa tatu Raila Odinga Junior wengi wanaamini ni jina la babake lakini Mama Ida amekosoa hilo akisema alimpa jina la somo yake aliyefahamika kama Raila Kembo.
Winnie Odinga ambaye ni kitinda mimba, jina lake lilitokana na mke wa kiongozi mpiganiaji uhuru nchini Afrika Kusini Nelson Mandela Winnie Mandela.
Mama Ida alielezea kwamba akiwa hospitali akisubiri kujifungua mtoto wake wa mwisho alikuwa akitizama runinga na wakati huo, Mandela akawa anaachiliwa huru kutoka gerezani.
Anasema akiwa kitandani aliona Mandela akitoka kwenye malango ya gereza akiwa amemshika mkono mke wake Winnie Mandela, na tayari akawa amepata jina la mwanawe.