Mama Ida ahimiza amani katika maombolezi ya Raila Odinga

Marion Bosire
2 Min Read

Mjane wa marehemu kiongozi wa muda mrefu Raila Amolo Odinga, Mama Ida Odinga amehimiza wananchi kwa jumla kutanguliza amani hata wanapomwomboleza kiongozi waliyempenda ambaye ni mume wake.

Akizungumza katika uwanja wa Nyayo wakati wa ibada ya wafu kwa ajili ya mume wake, Ida alisema kwamba iwapo kuna kitu ambapo Raila alipenda na alihimiza kila mara ni amani.

Ida alianza kwa kuelezea kwamba ana jina refu sana na mengi ya majina hayo hayaji bure tu bali yana majukumu makubwa.

Mojawapo ya majina hayo ni balozi wa amani yaani “Peace Ambassador” akisema mume wake alisimamia amani ambapo alisema kila mara kwamba amani inahitajika sana katika nchi yetu na katika kiwango cha familia.

Mkewe Raila anasema katika siku zake za mwisho mwisho, Raila alisisitiza sana kuhusu haja ya kuhimiza wakenya kuishi pamoja kwa amani.

Ida alisema kwamba anafahamu fika jinsi waliompenda Raila wana huzuni na wanamwomboleza lakini akasisitiza kwamba ni sharti washikilie amani wakati huu wa maombolezi.

Kando na hayo, Mama Ida alisema kwamba leo ni siku ya kipekee kwani sio kila siku anasimama mbele ya umma kuzungumza kuhusu mume wake mpendwa Raila Amolo Odinga.

Mama Ida alizungumzia pia jambo jingine alilolipenda Raila ambalo ni kusamehe akitoa mfano wa jinsi aliwania Urais mara kadhaa, majibu yakawa na utata lakini akatanguliza msamaha.

Ndiposa anawasihi wakenya kwamba wasiweke chuki kwenye mioyo yao kwani sote ni wakenya, ndugu na dada tunaostahili kushikamana kusongesha taifa mbele.

Hakusahau pia kutaja mambo ambayo Raila hakuyapenda katika maisha yake kama vile uwongo na ulafi ambao anasema umechochea wengi walio kwenye uongozi kufuja raslimali za umma.

Share This Article