Mama mmoja na rafiki yake wamekamatwa na polisi kuhusiana na kifo cha mwanawe wa kiume wa umri wa miaka minne.
Mama huyo kwa jina Melvin Owuor ambaye ni mama mzazi wa mtoto huyo akiwa na rafiki yake wanaripotiwa kupeleka mwili wa mtoto huyo katika makafani ya hospitali ya Mama Lucy Disemba 9, 2024.
Wawili hao walikosa kurejea siku hiyo baada ya kupiga ripoti ya tukio hilo kwa maafisa wa polisi walivyoagizwa na wasimamizi wa chumba cha kuhifadhi maiti.
Melvin na rafiki yake walizima simu zao, hatua iliyoacha wasimamizi wa makafani na maswali mengi, wakaamua kuripoti tukio hilo katika kituo cha polisi cha Mowlem.
Maafisa wa upelelezi kutoka Dandora na wenzao wa Nairobi walianza kushughulikia kesi hiyo na uchunguzi wao ulifichua mengi ya kushtua kuhusu nyakati za mwisho za uhai wa mtoto huyo.
Mshukiwa alisema kwamba mtoto alifariki akiwa amelala lakini uchunguzi ulibaini kwamba alifariki kutokana na majeraha aliyosababishiwa na mamake.
Inaripotiwa kwamba mtoto huyo alijinyea mama akakasirika na kumwadhibu vikali.
Mshukiwa wa mauaji hayo ataendelea kuzuiliwa kwenye seli za polisi huku uchunguzi ukiendelea ili kufahamu zaidi kuhusu kifo cha mtoto huyo.