Maluki azindua azma kuwania Urais wa NOC-K

Dismas Otuke
2 Min Read

Kinara wa Kenya, Shirikisho la Mchezo wa Judo Shadrack Maluki, ametangaza azma ya kuwania Urais wa Kamati ya Olimpiki nchini Kenya, NOC-K, kumrithi Dkt. Paul Tergat anayestaafu baada ya kuhudumu kwa kipindi cha mihula miwili.

Maluki, ambaye kwa sasa ni Makamu Rais wa kwanza wa NOC-K, ambapo amehudumu kwa miaka minane, amesema anawania kiti hicho cha urais akilenga kuboresha maslahi ya wanamichezo, kudumisha uadilifu, uongozi jumuishi, na usimamizi bora wa fedha.

Aidha, Maluki ambaye ni Rais wa Shirikisho la Judo barani Afrika, ameanzisha pia kikosi chake cha wawaniaji wa nyadhfa mbalimbali kwenye mrengo wake alioupa jina la ‘New Dawn Fresh Nock’.

Mwenyekiti wa riadha ya vijana Barnaba Korir, anawania kiti cha Naibu Rais wa kwanza, huku kinara wa chama cha Magongo Nahashon Randiek, akigombea wadhifa wa Naibu Rais wa pili.

Kinara wa chama cha Table Tennis Andrew Mudibo, anawania wadhfa wa Katibu Mkuu huku mwenzake wa Soft Ball, Francis Karugu, akigombea wadhifa wa Katibu Mkuu. Mwenyekiti wa mchezo wa Fencing Fred Chege, anawania kuwa mtunza hazina huku Charles Mose wa Shirikisho la Uendeshaji Baiskeli akiwania kuwa Naibu Mtunza Hazina.

Bingwa mara mbili wa Olimpiki katika marathon Eliud Kipchoge, anawania kiti cha mwakilishi wanamichezo wakati Lilian Mududa, Joyceline Nyambura na Rais wa Chama cha Raga nchini Sasha Mutai, wakiwania viti vya wanachama wa kamati kuu.

Wajumbe 29 kutoka mashirikisho ya michezo nchini yaliyo katika mwavuli wa NOC-K yatapiga kura tarehe 24 mwezi huu.

Share This Article