Mali Safi Chito asema amerejea nyumbani

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Kenya Milycent Jerotich Kipkorir maarufu kama Marakwet Daughter, mwimbaji wa kibao maarufu cha “Mali Safi Chito” amesema kwamba sasa amerejea nyumbani.

Jerotich alichapisha picha za pamoja na mbunge wa eneo la Kapseret katika kaunti ya Uasin Gishu, Oscar Sudi kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii na kuziambatanisha na ujumbe huo.

Mwimbaji huyo alikuwa amevaa mavazi ya rangi za chama tawala UDA ambazo ni manjano na kijani.

“NIMERUDI NYUMBANI NINAPOSTAHILI KUWA”  Ndiyo mada aliyochagua mwanamuziki huyo kwa ujumbe wake ambapo alielezea kwamba kama msanii wa muziki, safari yake imekuwa na changamoto nyingi.

“Wakati mwingine, misukosuko imenipoteza njia au kusababisha nikaudhi mashabiki wangu bila kukusudia. Lakini nimeendelea kuwa na mtazamo wa mbele na kama Mali Safi Chito, nimejitolea kuwaletea mashabiki wangu vibao vikali mfululizo” alisema.

Milycent alihakikishia mashabiki zake kwamba hakuwa amepotea huku akiomba msamaha kutoka kwa yeyote aliyemkwaza katika mapito yake.

Sudi naye alichapisha picha hizo akisema, “Kama baba, huwa ninakaribisha waliopotoka nyumbani. Ninawaalika na kuwatengenezea nafasi”.

Kiongozi huyo aliendelea kusema kwamba nyumba yake kama baba ni kubwa na ina nafasi ya kila mmoja huku akimkaribisha Milycent nyumbani.

Haya yanajiri saa chache baada ya uvumi kusambaa kwamba msanii huyo ambaye alilalamikia kutengwa na chama tawala anapitia magumu na amelazwa hospitalini.

Wakati mmoja msanii huyo alichapisha video iliyokuwa na ujumbe mzito kwa Rais William Ruto ambao ulizua minong’ono mitandaoni.

Wimbo wake “Mali Safi Chito” ulimpa umaarufu lakini hali hiyo ilionekana kubadilika haraka.

Share This Article