Kiongozi wa chama cha Economic Freedom Fighters – EFF nchini Afrika Kusini Julius Malema amepatikana na hatia katika kesi inayohusu silaha ambapo alifyatua risasi hadharani katika tukio la miaka saba iliyopita.
Kosa hilo lina hukumu ya hadi miaka 15 gerezani na anadaiwa kulitekeleza mwaka 2018, ambapo alifyatua risasi kadhaa hewani wakati wa shere ya kuadhimisha miaka mitano ya chama hicho katika mkoa wa Eastern Cape.
Malema alishtakiwa pamoja na aliyekuwa mlinzi wake wa kibinafsi Adriaan Snyman, ambaye aliondolewa lawama katika kesi hiyo.
Haya yanajiri chini ya miezi miwili tangu Malema alipopatikana na hatia ya kutoa matamshi ya chuki yaliyolenga wazungu ambao ni wachache nchini Afrika Kusini.
Malema katika usemi huo alitaka wazungu hao wapokonywe mashamba wanayomiliki na mali zao kuhamishiwa raia weusi wa Afrika Kusini.
Katika kesi ya hivi punde Malema alipatikana na hatia katika makosa matano yakiwemo kuwa na silaha bila kibali, kufyatua risasi hadharani na kuhatarisha maisha ya watu bila kujali.
Risasi alizofyatua siku hiyo zinakisiwa kuwa kati ya 14 na 15 akiwa jukwaani mbele ya wafuasi wengi wa chama cha EFF.