Malala atakiwa kujisalimisha kwa polisi

Tom Mathinji
1 Min Read
Naibu kiongozi wa chama cha Democracy for the Citizens (DCP) Cleophas Malala. Picha/Hisani.

Naibu kiongozi wa chama cha Democracy for the Citizens (DCP) Cleophas Malala, amepewa saa 71 kujisalimisha kwa  polisi la sivyo atakamatwa atakapoonekana.

Malala anahitajika kuhojiwa kuhusiana na ghasia za Jumamosi zilizogubika mkutano wa chama hicho katika kaunti ya Kakamega, ambapo magari yake matatu yalinaswa na maafisa wa usalama.

Akizungumza afisini mwake, kamanda wa polisi wa eneo la Magharibi Issa Mohammud alisema Malala hakuwajulisha polisi kuhusu mkutano wake wa kisiasa kama inavyohitajika kisheria.

Mohammud alimshutumu Malala kwa kutatiza usalama mjini Kakamega na kwamba atashtakiwa na kosa hilo pindi tu atakapokamatwa.

Mkuu huyo wa polisi eneo la Maghribi aliongeza kuwa Seneta huyo wa zamani atashtakiwa na kosa la uendeshaji mbaya wa gari uliotishia maisha ya raia, kutatiza waendeshaji magari wengine na kukiuka kanuni za trafiki.

Tayari washukiwa 18 wamekamatwa kuhusiana na zogo la siku ya Jumamosi.

Share This Article