Makubaliano kati ya JKIA na Adani kusitishwa kwa wiki mbili

Martin Mwanje
2 Min Read

Utata unaozingira ukodishaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA ulizidi kutokota huku makubaliano kati ya JKIA na kampuni ya Adani yakisitishwa kwa muda wa wiki mbili. 

Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji ya Umma ya Bunge kuhusu Masuala ya Biashara na Nishati David Pkosing amesema hatua hiyo imechukuliwa ili kumpa fursa Mkaguzi Mkuu wa serikali Nancy Gathungu kupigia darubini makubalinao hayo.

Akizungumza wakati wa kikao cha kamati hiyo na maafisa wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini, KAA katika majengo ya bunge leo Jumanne, Pkosing ameonya kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya KAA ikiwa itasonga mbele na utekelezaji wa makubaliano hayo kabla ya utata unaozingira makubaliano hayo kusuluhishwa.

Alisema punde watakapopokea ripoti ya Mkaguzi Mkuu baada ya kipindi cha siku hizo 14 za ukaguzi, wataiambatanisha kwenye mapendekezo yao na kisha kuiwasilisha bungeni.

Ni wakati huo ambapo bunge linatarajiwa kutoa mwelekeo wa makubaliano kati ya JKIA na kampuni ya Adani ya India.

Wakati huohuo, Waziri wa Fedha John Mbadi amesema kuwa yeyote aliye na shauku ya kuingia katika makubaliano ya kustawisha uwanja wa JKIA yuko huru kuwasilisha mapendekezo ya kustawisha uwanja huo.

Makubaliano ya kukodi uwanja wa JKIA kwa kampuni ya Adani kutoka India kwa kipindi cha miaka 30 yamezua mdahalo mkali huku wengi wakihoji kukodishwa kwa uwanja huo katika kipindi cha miaka 30.

Wafanyakazi wa KAA wamepinga vikali makubaliano hayo kwa hofu ya kupoteza ajira.

 

 

 

 

Share This Article