Makamu mwenyekiti wa CHADEMA bara amtetea Lissu

John Heche alikuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Aprili 23,2025, ambapo alimtaja Rais Samia kwani kesi ni yake akimtaka aiondoe mahakamani.

Marion Bosire
2 Min Read
John Heche.

Makamu Mwenyekiti wa chama cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA maeneo ya bara, John Heche amemtetea kiongozi wa chama hicho Tundu Lissu akisema yeye sio mhaini.

Kutokana na hilo, Heche anaitaka serikali ifute kesi ya uhaini inayomkabili mwenyekiti huyo wa CHADEMA akisema ni kesi ya uongo.

Heche alikuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Aprili 23,2025, ambapo alimtaja Rais Samia kwani kesi ni yake akimtaka aiondoe mahakamani.

“Wamfutie Lissu kesi ya uongo ya uhaini kwa sababu Lissu sio mhaini, huwezi kufanya uhaini ukiwa raia ambaye hajawahi kuwa na kikundi cha kijeshi, hana kikundi cha kijeshi anachokiongoza, hawawezi kuthibitisha popote mwisho wa siku itakuwa kesi kama ya Freeman Mbowe” alisema Heche.

Makamu huyo wa mwenyekiti aliendelea kushangaa jinsi viongozi wa CHADEMA wamefunguliwa mashtaka chini ya uongozi wa Rais Samia ambaye amehudumu kwa muda ulio chini ya miaka minne.

“Alijaribu kumfungulia kesi ya ugaidi mwenyekiti Mbowe ambayo hukumu yake ni kunyongwa mpaka kufa, amejaribu tena kumfungulia Lissu kesi ya uhaini ambayo hukumu yake vilevile ni kunyongwa mpaka kufa” alisema Heche.

Kesi dhidi ya Lissu inatarajiwa kuendelea kesho April 24,2025 katika Mahakama ya Kisutu jijini Dar es salaam ambapo Heche amewataka Watanzania wote wajitokeze kwa wingi kuifuatilia.

Lissu alikamatwa tarehe tisa mwezi huu wa Aprili baada ya mkutano wa kisiasa katika eneo la Mbinga, Kusini mwa Tanzania katika kampeni ambayo chama chake kimekuwa kikiendesha ya kuhimiza mageuzi kabla ya uchaguzi.

Alhamisi Aprili 10, 2025 alifikishwa katika mahakama ya Kisutu ambapo hakukubaliwa kula kiapo kuhusu kosa la uhaini lakini alikanusha shtaka jingine la kusambaza habari za uwongo.

Share This Article